Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Video ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP inaonesha roboti watatu wakiwa wamefungwa vifaa viwili vinavyomwaga dawa ya kuua vijidudu, kupima joto la mwili, kufuatilia, kutunza taarifa za abiria pamoja na usimamizi wa wagonjwa.
Mwakilishi mkazi wa UNDP nchini Kenya Walid Badawi anasema majina ya roboti hao watatu ni Jasiri, Tumaini na Shujaa.
“Mwanzoni mwa janga hili la Corona UNDP tulitoa fursa ya kusaidia ulimwengu kulingana na maono yetu kama shirika la maendeleo katika maeneo ya kujiandaa, kukabiliana na kupona changamoto zilizoletwa na janga hili”, amesema Bwana Badawi.
Watendaji kadhaaa katika uwanja huo na halikadhalika Hospitali Kuu ya Kenyatta jijini Nairobi wamepatiwa mafunzo ambapo Dkt Amina Guleid ni mwenyekiti wa kamati ya kusimamia programu hii ya roboti na anasema, “mpaka sasa tumeshawafundisha wataalamu wetu watano wa TEHAMA namna ya uendeshaji wa roboti hawa, na tunaendelea na watoa huduma wengine wa afya, na madaktari ambao watatoa ushauri wa kitaalamu kwenye masuala ya kliniki. Lakini pia tunaye mtaalamu wa afya ambaye anahusika kwenye eneo la kufukiza dawa na ndio anatuongoza namna sahihi ya kufukiza.”
Roboti hao pia wanaepusha wahudumu wa afya kuwa karibu na abiria na hivyo kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya Corona.
Utaalamu huo wa kutumia roboti umebuniwa na kampuni ya Zorabots Afrika Limited chini ya ufadhili wa UNDP Rwanda, na Mkurugenzi mtendaji wake Benjamin Kerenzi anasema roboti hao wana uwezo wa kuchakata takwimu na kutoa taarifa wakati huo huo, hivyo kuwasaidia wafanya maamuzi kuwa na taarifa sahihi.../
342/